Thursday, August 18, 2011

BAADA YA NGAO YA JAMII (TFF) KUZISHITAKI SIMBA NA YANGA

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ina msimamo wa  kuzishitaki Simba na Yanga kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya shirikisho hilo, kutokana na matamko yaliyotolewa na viongozi wa klabu hizo siku chache kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa jana.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kauli zilizotolewa na Simba na Yanga kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii, zinarudisha nyuma mipangilio ya maendeleo ya soka ya Tanzania.

Osiah alisema kabla ya suala hilo kufikishwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi, Kamati ya Utendaji ya TFF itaketi kuzungumzia kauli zilizotolewa na viongozi hao.

“Sekretarieti itaketi na ikibainika kauli zilizotolewa ni matakwa ya viongozi ama ni matamshi ya baadhi yao na si makubaliano ya klabu, viongozi wa klabu watatakiwa kutetea matamshi yaliyotolewa, la sivyo hatua zitachukuliwa,” alisema Osiah.

Aidha, Osiah alisema katika mchezo huo amejitokeza mdau ambaye ni Kampuni ya Big Bon aliyenunua mechi hiyo ya Simba na Yanga kwa sh milioni 300.

Osiah alisema, Simba walipiga kelele kuhusu usajili wa mchezaji wa kimataifa, Gervais Kago, ambaye usajili wake haujamilika, huku Yanga nao badala ya kujipanga kwa mchezo wa jana, wakaanza kupiga kelele kuhusu fedha za ruzuku walizotakiwa kupewa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup).

Alisema pamoja na kumruhusu Kago kucheza mchezo wa jana, lakini hatacheza Ligi Kuu kwa sababu taratibu zake za uhamisho hazijakamilika.

Katika hatua nyingine, Osiah alisema kuhusu zawadi ya kipa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Yaw Berko, suala hilo liko mikononi mwake, kwa sababu TFF bado ina matatizo ya fedha.

No comments:

Post a Comment